TAMATI YA MTUNZI


TAMATI YA MTUNZI.
Josephat S. Hema

Laiti ningalijua,kutunga japo utenzi,
Sifa ningemwagia,japo wengi wamuenzi,
Sana ningemsifia,alivyokuwa kipenzi,
Daima tamlilia,tamati yake mtunzi.

Pale alipoishia,alionesha ujuzi,
Kalamu akaachia,ilipomwishia pumzi,
Huku tukimwangalia,ilo bora yake kazi,
Wote tuliobakia,kumuiga hatuwezi.

Yale maneno sawia,aliyoyaweka wazi,
Wino katuandikia,kwa ukweli na uwazi,
Fahamu kutufungua,maarifa waziwazi,
Bado tunakumbukia,hayatuishi majonzi.

Kichwa busara sawia,alikua na makuzi,
Hata anayoongea,yamejaa uchunguzi,
Makini anang’amua,ni kama mpelelezi,
Zile siri azojua,ni za hatari baadhi.

Mioyo aliinua,kwa makala changanuzi,
Tumaini alitoa,kwa vizazi na vizazi,
Alitembea dunia,na kutoa fafanuzi,
Wale wanaokimbia,yanawatoka machozi.

Japo bado apumua,alishaiacha kazi,
Anasema inaboa,yamnyima usingizi,
Vitisho anapokea,awekapo mambo wazi,
Kaona kujiokoa,aache upaparazi.

Muwazi anapokua,kuna watu awaudhi,
Wako nyuma ya pazia,wanaleta vizuizi,
Vigogo akiumbua,aharibu yao kazi,
Hapo kilichofatia,ni tamati ya mtunzi.



No comments:

Powered by Blogger.