MFEREJI WA MAJI


MFEREJI WA MAJI
Josephat S. Hema


Ule mto wa neema,katikati ya kijiji,
Wenye wingi wa neema,daima twauhitaji,
Mto umejaa mema,ni matamu yake maji,
Mbona sasa unakwama,huku kwetu hauji?

Siku sasa zayoyoma,tumepungukiwa maji,
Serikali wanasema,tatizo ni la kijiji,
Eti miti tunachoma,tukitafuta mtaji,
Hili linatupa homa,bora kingine kipaji.

Ila watu wanasema,kumezuka mfereji,
Wajanja walishapima,katikati ya kijiji,
Hapo mali wanachuma,kiwe chanzo cha ulaji,
Sie namba tunasoma,wao wanajifariji.

Viongozi wamezima,huku maji yanaisha,
Hata tunapolalama,wanasema tunachosha,
Tumekosa pa kusema,tumebaki sikitisha,
Hata kama tukisema,tamaa watukatisha.

Tunataka mtaalamu,wa kufanya utafiti,
Mfereji wa hujumu,inapasa kudhibiti,
Hili swala la muhimu,tukomboe wakati,
Lisije likawa sumu,tukakosa uthabiti.


No comments:

Powered by Blogger.