TANZANIA NAKUPENDA


TANZANIA NAKUPENDA
Josephat S. Hema





Tanzania nakupenda,moyoni umeingia,
Hata njaa nikishinda,wapi nitakimbilia?
Uzalendo ninalinda,hata kama ninalia,
Kuna muda wanishinda,nami binadamu pia.

Kwanza nilitafakari,kwa marefu na mapana,
Jinsi ulivyo mzuri,kama kasoro hauna,
Japo nawe una shari,ila sio nyingi sana,
Moyo ukanishauri,nyumbani kutulizana.

Tumepewa utulivu,wa miaka na miaka,
Hatujapewa makovu,sisi tulisalimika,
Wala si mengi maovu,wengi wamestaarabika,
Ila wapo na wavivu,japo wanahesabika.

Namkumbuka mwalimu,alivyotuunganisha,
Dini kabila ni sumu,sisi wamoja maisha,
Kila mtu wa muhimu,umoja kufanikisha,
Tukapata na elimu,japo mwanzo haikutosha.


Huko nje nikienda,Tanzania nitarudi,
Kuna baridi huenda,muda fulani lazidi,
Ubaguzi sitapenda,ule wa kimakusudi,
Nyumbani wananipenda,upendo ninafaidi.

Mkacha kwao mtumwa,alishasema mwalimu,
Hili jambo linasemwa,tena mnalifahamu,
Ya nini kuwa mtumwa?Nitabaki humu humu.
Hata kama nikiumwa,unazo tiba muhimu.

Sikuachi Tanzania,nasema hili kwa wazi,
Hili nimeshaamua,sibadili maamuzi,
Wale mnaokimbia,hata kwa kupiga mbizi,
Nashauri kubakia,tuzijenge zama hizi.


No comments:

Powered by Blogger.