WEMA
WEMA.
Josephat S. Hema
Ndugu siku zinaenda,kamwe hazirudi
nyuma,
Tazama unayotenda,usijepata lawama,
Ujitahidi kupenda,tena uwe na
hekima,
Je hili litakushinda?vipi ni
gharama wema?
Wengine walijikuta,mioyo inawauma,
Siku zilipowapita,wakidhani ni
gharama,
Kumbe muda ni ukuta,bora ufanye
mapema,
Mbona bado una siku?vigumu kutenda
wema?
Nyumbani unaanzia,kabla ya mbali
kufika,
Jirani anaanzia,kuupata uhakika,
Taratibu husambaa,na kuivuka
mipaka,
Wema unapoongea,Dunia yatikisika.
Wengine wanadhania,nguvu nyingi
hutumika,
Kwamba utagharamia,jambo jema
kufanyika,
La hasha ninakwambia,huko ni mbali
kufika,
Japo tabasamu toa,yu mtu afarijika.
Jiamini kwa kidogo,nguvuye huwezi
jua,
Hata kama ni kidogo,kuna mtu
chamfaa,
Mwanzo huwa ni mdogo,vikubwa
vyafuatia,
Siupe wema kisogo,kuna watu waumia.
Upendo ndio kitovu,cha wema kwenye
dunia,
Mngekuwa watulivu,kama
tungezingatiaa,
Tusingetumia nguvu,migogoro kuamia,
Wema huwa msikivu,hekima anatumia.
Tunaishi kwenye ndoto,kuibadili
Dunia,
Wema utakuwa wito,kama
tumedhamiria,
Japo ni mengi mapito,wema
unavumilia,
Kama ni kuvuka mto,wema ni yetu mashua.
Sasa iwe changamoto,wema
kuupalilia,
Jambo hili sio zito,ni hatua
kuamua,
Sio
uamuzi toto,japo hilo natambua,
Kwa pamoja uwe moto,wema kwanza
tangulia.
No comments: