KIJIWENI

KIJIWENI
Josephat S. Hema


Ile mida ya jioni,
Tukutane kijiweni,
Tuongee ya moyoni,
Jua likishuka chini,
Tukapumzike nyumbani.

Ni baada ya shughuli,
Zilizotukabili,
Mchana wa jua kali,
Tukaichosha miili,
Hata na zetu akili.

Tuliacha familia,
Umma kuutumikia,
Na jamii nzima pia,
Uzalendo tangulia,
Kuipenda TANZANIA.

Sasa ifike jioni,
Pale mgahawani,
Na kahawa mezani,
Kilichojiri ni nini,
Hapa kwetu nchini.


Hii habari ya dola,
Kupanda kimasihara,
Ni juu kila mara,
Ndio chanzo cha hasara,
Na hizi zetu hasira.

Uchumi uliolala,
Na hizi kodi za hila,
Tumekosa uimara,
Sasa twaona madhara,
Hili jambo linakera.

Kazi tu ndio moto,
Japo nyingi changamoto,
Na mambo mengi ni ndoto,
Tunaishi kwa msoto,
Sio mambo ya kitoto.

Mpaka tunatawanyika,
Kahawa yamalizika,
Tena bila muafaka,
Kesho yatumainika,
Japo ni ngumu kufika.



Tutakutana na kesho,
Leo isijekua mwisho,
Kuishi si hitimisho,
Kesho tena mipasho,
Kijiwe kisiwe michosho.

Hapa ndio kijiweni,
Kwa habari za mjini,
Hata kote duniani,
Na zile mpirani,
Kesho tena karibuni.

No comments:

Powered by Blogger.